RC Mtwara amtupa selo Afisa kiwanda cha Dangote
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, amemwagiza kamanda wa polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya kumuweka ndani ofisa kazi wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Nadhiru Omary kwa madai ya kushindwa kutatua malalamiko ya wafanyakazi ambayo yanaelekezwa katika ofisi yake.
Byakanwa ametoa maagizo hayo leo Jumatano, Jana Machi 7, alipofika kiwandani hapo baada ya baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho kugoma kuendelea na kazi kwa muda usiojulikana kwa madai mbalimbali.
Wafanyakazi hao wanadai kunyanyaswa, kutolipwa mishahara yao kwa wakati na kufukuzwa kazi bila kuzingatia sheria.
“Tangu nimefika hapa wewe bwana umelaumiwa na umetuhumiwa kwa mambo mengi,hata vikao vyote tulivyokaa hujabadilika, kwa sababu kama ungebadilika taarifa hizi tungezijua mapema,” alisema na kuongeza kuwa:
“Sisi kama Serikali tungekaa na watumishi hawa kabla hawajaanza kuandamana, RPC huyu akapumzike kwanza, kamata huyu mtu tuondoke naye hatuwezi kuendelea na watu ambao badala ya kusikiliza malalamiko ya watu.”
“Kama unakaa sehemu ya kazi halafu chama cha wafanyakazi hakipo na ofisa kazi hauchukui hatua zozote unapoteza sifa zote, inaonekana ni tatizo la kudumu na ni tatizo sana.”
Mhasibu idara ya usafirishaji kiwandani hapo, Justie Fumbuka ameiomba Serikali kuchunguza utaratibu wa utoaji vibali vya kufanya kazi na kuishi nchini kwa kuwa umegubikwa na rushwa inayotolewa kwa watendaji wa idara ya kazi na Uhamiaji wasiokuwa waadilifu.
“Mchakato uchunguzwe kwani vibali vimekuwa vikitolewa kwa wasio na sifa na ni wanyanyasaji wa wafanyakazi na tunaiomba Serikali iwaondoe nchini mara moja,” ameeleza Fumba mbele ya mkuu wa mkoa.
Machi 3 mwaka huu, waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alitembelea kiwandani hapo na kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho na baadaye alikutana na baadhi ya wafanyakazi wakiwamo madereva.
Wafanyakazi hao walimpa malalamiko yao ambapo aliahidi yatafanyiwa kazi baada ya kiwanda hicho kuanza uzalishaji Machi 15.
READ MORE https://www.jamiiforums.com/threads/rc-mtwara-amtupa-selo-afisa-kiwanda-cha-dangote.1410578/
Comments
Post a Comment