RPC Susan Kaganda adai hakutoa maelekezo ya kuzuia mkutano wa Nape
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni Susan Kaganda, amesema kuwa yeye hakutoa maelekezo ya kuzuia mkutano wa aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Nape Nnauye pamoja na Waandishi wa Habari Jana Protea Hotel.
Akifafanua kupitia kipindi cha Maisha Mseto cha Times Fm mapema Leo asubuhi, Susan amedai yeye kama Kamanda hana mamlaka ya kuingilia biashara binafsi (Protea Hotel), na alikwenda pale kuhakikisha Usalama unaimarika zaidi na si vinginevyo.
“Protea ni private Hotel sio Mali ya Serikali, ile ni Biashara huru kamanda hawezi kuzuia, lakini nilikuta Waandishi wengi pale na alipata fursa ya kuongea nao.
” Mimi kazi yangu ni kusimamia Usalama wa Raia na Mali zao, mkutano unanihusu ukiwa wa Hadhara” alisema RPC Susan.
Alipoulizwa kuhusiana na kipande cha ‘Picha Jongefu’ (video) inayomuonyesha mtu anayedhaniwa kuwa Askari akimtolea silaha Nape Nnauye, amesema hawezi kuliongelea swala hilo kwa sasa mpaka uchunguzi utakapokamilika kwa maana kipande hicho hakionyeshi Sura ya mtu Huyo.
“Jeshi la Polisi tunawafundisha Askari wetu kutumia nguvu kwa namna wanavyokutana na mazingira, sikuwepo sikuona nilielezwa na ndio maana nilikwenda nikamuuliza Mh uko sawa akanijibu yuko salama,”
“Lakini kama kuna Silaha imetumika kama ambavyo nimeona kwenye vyombo vya Habari tunalifanyia Uchunguzi, sikuwepo eneo la tukio picha ile inaonyesha KISOGO, kuwa mtulivu tunachunguza” alifafanua.
Comments
Post a Comment